Mbeya City yaishusha Yanga kileleni

 




Klabu ya Mbeya City imeishusha Yanga kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu NBC baada ya kuifunga Dodoma Jiji mabao 3-1 katika mchezo uliochezwa kwenye uwanja wa Liti mkoani Singida.

Kwa matokeo hayo Mbeya City  imepanda kileleni mwa msimamo  kwa kuwa na  mabao matatu ya kufunga na moja la kufungwa  huku Yanga  ikibaki na mabao mawili ya kufunga na moja la kufungwa.

Katika mchezo huo mabeki wa Dodoma Jiji walikuwa na makosa mengi yaliyowapa nafasi Mbeya City kuweza kupata mabao hayo matatu.

Kiungo wa zamani wa Dodoma Jiji ambaye kwa sasa anaichezea Mbeya City, Hassan Maulid aliwapoteza vilivyo waajiri wake hao wa zamani na kulishika vilivyo dimba akishirikiana na George Sangija.

Bao tamu lilikuwa la tatu la mshambuliaji  Eliud Ambokile ambaye alimalizia krosi ya Sixtus Sabilo dakika ya 63, ambaye aliwapiga chenga mabeki wa Dodoma Jiji na kisha kupiga krosi kwa mfungaji.

Dodoma iliuanza mchezo kwa kasi na dakika ya 18 ilipata bao la kuongoza   kupitia kwa Paul Peter kwa shuti kali akimalia kazi nzuri ya Seif Karihe.

ADVERTISEMENT

Baada ya bao hilo Dodoma ilifanya mabadiliko ya kumtoa Muhsin Malima na nafasi yake kuchukuliwa na Salmin Hoza dakika ya 20.

Mbeya City ilikuja juu na kufanikiwa kusawazisha bao hilo  dakika ya 26  baada ya Rashid Mohammed   wa Dodoma Jiji kujifunga katika harakati za kuokoa.

Mchezaji wa zamani wa Namungo Sixtus Sabilo aliifunga bao la pili Mbeya City dakika ya 42 kwa kichwa akimalizia krosi ya Eliud Ambokile.

Hadi mapumziko washindi walikuwa mbele kwa mabao 2-1 ambapo kipindi cha pili Dodoma Jiji walikianza kwa kasi lakini kipa wa Mbeya City Harun Mandanda alikuwa makini kuokoa michomo ya washambuliaji wa Dodoma Jiji, Seif Karihe na Paul Peter.

Dakika ya 49  kipa wa Dodoma Jiji Aron Kalambo alikoa michomo ya washambuliaji wa Mbeya City, Tariq Seif na Sixtus Sabilo.  

Kocha wa Dodoma Jiji,Masoud Djuma  alifanya mabadiliko ya kuwatoa Jimmy Shoji, Paul Peter, Rashid Mohammed na Hassan Kessy na  nafasi zao zilichukuliwa na Habib Seif, Hassan Mwaterema,  Enrick Nkosi na Anderson Kimweri.

Kwa upande wa Mbeya City walimtoa Tariq Seif na nafasi yake kuchukuliwa na Gasper Mwaipasi.

Hata hivyo mabadiliko hayo hayakubadilisha matokeo hayo kwani hadi fimbi ya mwisho ya mwamuzi Ally Mnyope kutoka Morogoro  Dodoma Jiji ilikubali kichapo cha mabao 3-1.

Katika mchezo huo mwamuzi Mnyope aliwapa kadi za njano George Sangija wa Mbeya City na Muhsin Malima na Hassan Kessy wa Dodoma Jiji kutokana na mchezo  ambao sio wa kiungwana.

Post a Comment

Previous Post Next Post